Ripoti Ya Afisa Mkuu Mtendaji Wa Kampuni

Ukanda wa Afrika Mashariki ulipata afueni ya kiuchumi kutoka kwa athari kubwa ya tandavu ya UVIKO-19 huku ukuaji wa wastani wa 7.5% wa Pato la Kawaida la Taifa ukiwa wa -0.3% mnamo 2020. Kurejea kwa hali ya kawaida katika ukanda huu kulitokana na kurejea kwa shughuli za utalii, kuimarika kwa bei za bidhaa na hitaji la bidhaa kote duniani, mavuno ya kutosha kutokana na kilimo pamoja na kuondolewa kwa masharti yaliyokuwa yamewekwa wakati janga hili lilipoanza ili kudhibiti kuenea kwa tandavu ya Covid-19. Kuzinduliwa kwa chanjo kwa kila mtu kote barani na kuimarika kwa uzingatiaji uliokuwa umewekwa katika sekta ya uchumi dijitali kulichukua nafasi muhimu katika kurejea kwa ukuaji wa ukanda huu, ingawa ukuaji huu haukufanyika kwa usawa katika sekta zote huku sekta kama vile ya utalii ikiwa bado chini ya shinikizo.

Kadhalika, sekta ya uanahabari ilishuhudia ukuaji japo kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na 2020, kutokana na kulegezwa kwa vikwazo vya usafiri na kufunguliwa kwa uchumi. Hatua hizi zilidhibiti mitindo ya matumizi ya bidhaa katika masoko na kuruhusu biashara mbalimbali kuendesha kampeni za bidhaa na huduma kote kwenye majukwaa ya machapisho, matangazo na dijitali ili kuendesha uhamasishaji wa bidhaa pamoja ukubalifu wake, jambo ambalo kwa upande mwingine lilisababisha athari chanya katika matokeo ya biashara yetu.

Hata hivyo, mafanikio yaliyopatikana mwaka wa 2021 yanakabiliwa na changamoto ya kuzoroteshwa kutokana na janga linaloendelea nchini Ukraine pamoja na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi vikitarajiwa kuwa na athari mbaya zaidi kwa bei ya vyakula, mafuta na bidhaa nyinginezo muhimu pamoja na usambazaji wa bidhaa kote duniani.

Matokeo ya Kifedha

Faida ya Kampuni kabla ya ushuru ilikuwa bilioni 0.7, ilikuwa juu kuliko mwaka uliopita. Hali ya kurejea kwa biashara iliyoanza katika nusu ya pili ya 2020 baada ya uharibifu mbaya uliosababishwa na Covid-19 ilidumu katika mwaka wa 2021 kwa sababu kuu kwamba kulikuwa na ukuaji katika matangazo kupitia televisheni na machapisho, matangazo ya kidijiali na usajili katika Gazeti la mtandaoni (E-paper).

Kuendelea kurejea kwa matangazo ya machapisho kumepigwa jeki na kurejea polepole kwa shughuli za kiuchumi kote katika ukanda huu. Ili kuyazungumzia matokeo haya chanya ni kwamba, usajili katika Gazeti letu la mtandaoni umeendelea kukua huku tabia za matumizi ya maudhui zikibadilika kuenda dijitali. Mikakati ya kudhibiti gharama na kuboresha biashara iliyozinduliwa wakati tandavu hii ilianza imesababisha kuimarika kwa ufanisi wa kuendesha biashara na kuendelea kuathiri upatikanaji wa faida na mtiririko wa pesa taslimu kwa njia chanya.

Safari ya Mageuzi ya Kidijitali

Mandhari ya vyombo vya habari yameendelea kukua na kubadilika katika miaka michache iliyopita na 2021 haikusazwa. Kuendelea kukumbatiwa kwa majukwaa ya kidijitali kwa matumizi ya maudhui kumetoa changamoto kwa majukwaa ya jadi ya habari na uzalishaji wao wa mapato, hii inamaanisha kwamba mashirika yamelazimika kupanga upya na kuoanisha miundo yao ya kuzalisha mapato. Kwa hivyo tumeendelea kuunda upya miundo ya biashara ya Kampuni hii kutoka muundo wa awali ya matangazo hadi kwa muundo wa mapato unaompa msomaji kipaumbele ili kuendelea kuendana na mabadiliko haya katika soko.

Kufuatia uzinduzi wa bidhaa kuu ya kidijitali ya shirika hili, Nation. Africa, NMG ilichukua hatua kubwa ya kuwa kampuni ya kwanza kabisa ya habari Afrika Mashariki na Kati kuzindua huduma ya kujisajili ili kupata maudhui ya habari kidijitali. Jukwaa la Nation.Africa paywall, lililozinduliwa mnamo Februari 2021, linalenga kufanya vyanzo vyetu vya mapato kuwa anuai, kuwapa wasomaji wetu uwezo wa kuchagua maudhui ambayo wangependa kutumia, kuchangia katika kutoa mwongozo kuhusu ajenda katika bara hili na kuimarisha ubora wa habari zinazozalishwa.

Ingawa uzinduzi wa jukwaa hilo la malipo ulipokelewa kwa hisia mseto katika soko, hadhira yetu ilianza kukubali kwamba katika karne hii, ni sharti mtu agharamike ili kupata maudhui bora. Jukwaa hili limesajili zaidi ya watumiaji binafsi 61,000 katika mwaka wa kwanza tangu kuzinduliwa kwake mnamo Februari 2021, huku takriban watumiaji 21,000 wakilipia kusoma habari zetu kila siku.

Tunafahamu ukweli kwamba safari ambayo tulianza ya kuchuma kutokana na habari itakuwa ni ndefu na yenye panda shuka nyingi, lakini tumejitolea kutoa maudhui ambayo yanafaa muda na pesa ya hadhira yetu; ambayo yanaakisi, yanavutia, mtu anaweza kujinasibisha na kujihusisha nayo.

Katika juhudi za kupiga hatua kufikia lengo letu la kuwa Chombo cha Habari cha Afrika kwa Ajili ya Afrika, pia tulizindua ukurasa wa Afrika uliotuwezesha kupanua maudhui na hadhira tunayoifikia barani na pia ughaibuni. Ukurasa huo unajivunia habari na hadhithi za hivi punde, zilizofanyiwa utafiti vyema na zinazofaa kwa hadhira zetu.

Mipango ya Utafutaji Soko
Katika mwaka uliopita, NMG ilizindua kampeni za kutafuta soko, matukio na shughuli za nyanjani kuendesha uhamasisho kuhusu bidhaa, mapenzi kwa bidhaa na kukumbatiwa kwa bidhaa kote katika ukanda huu.

Machapisho

Utafiti uliofanywa 2021 na Baraza la Wanahabari Kenya (MCK) ulionyesha kwamba gazeti la Daily Nation linalochapishwa na NMG linasalia kuongoza nchini huku washiriki wakiashiria kwamba gazeti hili ndilo chaguo lao. Ili kudumisha msingi wake katika kuongoza na kusisitiza nafasi ya bidhaa yake kama sauti ya wanyonge na mshirika wa kuaminika katika demokrasia ya Kenya, Daily Nation iliendesha kampeni ya “You Deserve the Truth”. Kampeni hiyo iliangazia taarifa za ukweli katika Habari za Kitaifa, Kaunti, Mtindo wa Maisha, Jinsia, Mazingira na Spoti, na kutoa changamoto kwa masuala ya kijamii na kiuchumi huku ikitumia kauli mbiu ya kampeni ya kuleta umoja ya “You Deserve the Truth”.

Kauli mbiu hiyo iliipa hadhira yetu kipaumbele katika kampeni na ililenga kuwavutia kwa bidhaa katika mazungumzo sehemu zote kwenye masoko, na kusababisha ufikiaji wa mitandao ya kijamii wa watu milioni 210. Kando na haya, Daily Nation iliendesha kampeni ya “Faulu na Nation”, iliyoandaliwa maalum ili kuanzisha uhusiano wa kihisia na wasomaji wetu ambao ni vijana pamoja na watu wazima, kwa kulirai taifa kutuma ujumbe wa kheri ya fanaka kwa watoto wanaofanya mitihani yao ya shule ya msingi na sekondari. Kupitia kampeni hiyo, Daily Nation ilichapisha zaidi ya ujumbe 300 na kufikia zaidi ya watumiaji milioni 5.5 wa mtandao wa kijamii.

Tuzo zilizosubiriwa kwa hamu za Business Daily’ za “Top 40 under 40” Wanaume na Wanawake zilirejeshwa tena 2021 baada ya kusitishwa kwa muda wa mwaka wa 2020 kutokana na tandavu ya Covid-19. Zikiwa ndizo za kwanza kabisa katika sekta ya habari nchini Kenya, tuzo hizo za kila mwaka zimeendelea na zinatambua watu nchini wanaofanya mabadiliko ambao wametoa mchango wa kipekee katika nyanja zao. Tuzo za 2021, ambazo zilipokea zaidi ya washiriki 2,000, zilivutia washiriki kutoka sekta mbalimbali kuanzia wanamuziki, wanariadha wanaoishi na ulemavu, madakatari wa upasuaji, wataalamu wa usalama mtandaoni, wahandisi wa ndege na wabunaji wasanifu wa 3D waliojifunza wenyewe.

Tuzo hizo zinaendelea kunasibishwa na ari, ufanisi na athari yake miongoni mwa watu wa umri, tasnia na taaluma mbalimbali. Tuzo za Top 40 Under 40 zimefungua nafasi za kazi na utambuzi wa kimataifa kwa washindi wa hapo awali, kwa sababu ya kuimarika kwa uaminifu wa biashara na mitandao kukua. Tuzo hizi zilichukua nafasi muhimu katika kuweka Business Daily kama chapisho la kutamanika na kuongeza kutegemeka kwake na hadhira lengwa.

Kutokana na kubadilika kwa mandhari ya uhariri, pamoja na mahitaji ya mtumiaji anayebadilika kila mara, NMG ilizindua safari ya kuiweka Taifa Leo, gazeti la pekee nchini Kenya linalochapishwa kwa Kiswahili, katika nafasi mpya, kama gazeti safi, la kisasa, ya kufahamisha, kuelimisha na kuburudisha lililojikita katika kupanua upeo wa Kiswahili ndani ya nchi na kimataifa. Hii ilisababisha kusanifiwa na kuzinduliwa upya kwa gazeti hilo ili kulipatia mwonekano jasiri, changamfu na safi, huku kwa wakati huo huo ikilifanya gazeti hilo kusomeka kwa urahisi. Uzinduzi huo, uliofanyika kwenye Kaunti ya Mombasa, ulituwezesha kusherehekea utamaduni tajiri wa Uswahili kupitia matumizi ya magwanda ya kitadamuni, mapambo na maonyesho ya vyakula vya Uswahilini.

Uzinduzi huo mpya ulisababisha ongezeko la 9.7% katika mauzo ya matoleo ya magazeti halisi ya Taifa Leo, na kufikia watu 15,228,365, na kuvutia hisia 184,561,465 kwenye mitandao ya kijamii na iliongoza miongoni mwa mambo yaliyovuma kwenye Twitter na kuchochea mazungumzo kuhusu lugha ya Kiswahili. Kadhalika, gazeti hili lilizindua Kampeni ya mikeka ya mezani katika mikahawa yaani Table Mats iliyotumika kwenye hoteli na maeneo ya maankuli kote nchini kuanzia ukanda wa Pwani, Kisumu, Kakamega, Eldoret, Nakuru na hadi Naivasha. Kampeni hiyo ililenga kulipigia debe gazeti hilo katika maeneo yaliyolengwa, kuongeza idadi ya watu wanaosoma toleo la ePaper kupitia kwa matumizi ya misimbo ya kutambaza ya QR iliyochapishwa kwenye mikeka hiyo. Kampeni hiyo ilidhihirisha ufanisi kukiwa na ongezeko la uhamasisho kuhusu gazeti hilo, kuongezeka kwa maswali kuhusu Taifa Leo na hoteli kugeuka kuwa mawakala wa gazeti hili ili kuendesha ufikivu wa gazeti hili katika eneo lao.

Mipango hii ya utafutaji soko ilifanya Taifa Leo kuwa chapisho linalokua kwa kasi zaidi nchini Kenya, ikiripoti ongezeko la 4.7% ikilinganishwa na 2020. Nchini Uganda, Monitor Publications Limited (MPL) ilizindua kampeni zenye kaulimbiu za kusherehekea Siku ya Wapendanao na Siku ya Kina Mama, huku washindi wakijishindia zawadi, mipango ya data ya kila mwezi na kutenga nafasi ya chajio ili kusherehekea na watumiaji wao Mwananchi Communications Limited (MCL) iliendelea kutumia Utafiti wao wa Mapendeleo ya Maudhui ili kupata maarifa kuhusu bidhaa zao na vitu vinavyovutia hadhira – mchakato wa kupokea maoni unaoendelea umekuwa muhimu kwa timu ya uhariri ili kuboresha maudhui yao, hususa ufuatiliaji wa habari za siku ya kwanza ya chapisho.

Kadhalika, wafanyikazi wa Tanzania walianza mchakato wa kuendesha mambo kidijitali na kusaidia utendaji wa kiuchambuzi wa habari ili kuleta suluhu za machapisho pamoja na utangazaji kwenye ukanda mzima. The Citizen ilizindua mipango mbalimbali ya kuhamasisha machapisho pamoja na matangazo ili kujiweka katika nafasi nzuri kama gazeti la biashara, mojawapo ya mipango hii ikiwa ni toleo la kwanza la Mpango wa Mwanamke Anayeinuka, chini ya kaulimbiu ya “Women in Leadership; Achieving an Equal Future” (Wanawake katika Uongozi; Kufikia Mustakabali wenye Usawa). Lengo la mpango huu lilikuwa ni kukuza viwango vya wanawake viongozi ili kuchukua nafasi muhimu katika asasi za umma na za kibinafsi ili kuchangia katika ukuaji wa biashara katika mandhari yanayobadilika kila wakati.

Ili kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania, MCL ilitumia majukwaa yake mbalimbali kuadhimisha hatua kubwa ambayo nchi iliyopiga. MCL iliangazia kampuni ambazo zimekuwepo kwa miaka hiyo 60, iliendesha kampeni za uchapishaji na kufanya maonyesho ya sekta tano kuu (Madini na Kawi, Fedha, Kilimo, Miundombinu na Elimu) ili kutoa makala ya hali halisi ya safari ya nchi hiyo kufikia Uhuru

Utangazaji kupitia Runinga na Redio

NTV Kenya ilidumisha nafasi yake kama kiamboni mwa burudani za spoti, kwa kupata haki za kipekee za kuonyesha mbio zilizosubiriwa kwa hamu za World Athletics Under 20 zilizoandaliwa nchini Kenya. Kando na hayo, NTV ilitia sahihi mkataba wa miaka mingi, wa ushirikiano wa kupeperusha matangazo na Shikirisho la Kitaifa la Mpira wa Vikapu (NBA), ili kutangaza mchezo wa All-Star na zaidi ya michezo 25 ya moja kwa moja katika nusu ya pili ya msimu wa 2020-2021. Kadhalika, NTV ilichangamsha mashindano ya Olimpiki ya Tokyo kwa kuyaonyesha kwa hadhira yao ya Kenya wakati wa michezo hiyo. Mkakati wa maudhui ya spoti uliendelezwa kwa stesheni yetu ya redio – Nation FM – ambayo mwaka jana ilizindua The Game Plan, kipindi cha kila wiki kinachoangazia na kujadili habari za spoti kutoka sekta mbalimbali.

Kuzinduliwa kwa kipindi hicho kulifanya stesheni hiyo ya redio kuandaa shughuli za nyanjani kote nchini ili kutoa hamasisho, kukuza jumuiya ya mashabiki wa spoti, kuboresha kupendwa kwa kituo hicho na kujiweka katika nafasi nzuri kama chaguo lao la stesheni ya spoti. NTV Kenya pia ilizindua vipindi vipya kama vile; With All Due Respect, kipindi kinachoangazia mazungumzo na mijadala na watu wanaogonga vichwa vya habari kuhusu masuala ya siku, na Attitude, kipindi cha muziki wa utamaduni wa pop ambacho kimevutia hadhira ya watu wachanga.

Dijitali

Ingawa Jukwaa la kujisajili la Nation. Africa paywall limekuwa likikua tangu kuzinduliwa kwake, kampeni fulani ilizunduliwa kama sehemu ya kampeni ya maadhimisho ya kwanza ya jukwaa hilo ili kugeuza watu wanaopita tu kwenye jukwaa hilo kuwa mashabiki sugu kupitia mchanganyiko wa mauzo kupitia barua pepe, majarida, maudhui ya kulipia, mauzo ya pamoja na zawadi za kidijitali. Kampeni hiyo iliwezesha ukuaji kwa 64% katika usajili na kuboresha uhamasisho na trafiki kwenye ukurasa wa Africa.

Kituo hicho pia kiliendesha Kampemi ya Kuandikishwa na Kujisajili iliyolenga kuunda uhamasisho wa juu na kuwasiliana kuhusu thamani ya uanahabari wa kina wa Nation. Africa na kuelimisha watumiaji kuhusu manufaa ya maudhui yanayolipiwa. Kampeni ya Africa & Diaspora iliyoendeshwa 2021, ililenga kutoa uhamasisho kuhusu ukurasa wa Africa kwa wasomaji wetu humu barani na ughaibuni ili kuwawezesha kufikia maudhui ambayo watu wanaweza kujinasibisha nayo. Kampeni hiyo ilisababisha ongezeko la uhamasisho nchini Afrika Kusini, Nigeria na Ghana, ikiongeza muingiliano faafu na hadhira katika masoko haya.

Nchini Uganda, Daily Monitor iliendeleza safari yake ya kufanya mambo kidijitali kwa kujiweka katika nafasi kama chapa inayoendeshwa kwa hisani ya Nation.Africa na iliendesha matangazo ya zawadi kwa lengo la kuongeza idadi ya watu waliojisajili mtandaoni kwa kuunda fursa za kushinda zawadi kama vile Televisheni, runulishi za watoto, vifaa vya kuhifadhi chaji ya simu, bidhaa zilizopigwa chapa na mengine mengi.

Matukio

Mwaka wa 2021, NMG iliandaa matukio kadhaa ya kushughulikia fursa za kushirikiana na washikadau na kuunda matumizi ili kuzindua upya bidhaa miongoni mwa hadhira yetu lengwa. Mojawapo ya matukio tuliyozindua katika kipindi hiki ilikuwa ni pamoja na Digital Summit, kongamano lililoandaliwa ili kutathmini mambo yanayovuma kidijitali barani Afrika na jinsi biashara zinaweza kuwasilisha thamani yao kwa washikadau wao. Tukio hili lilivutia zaidi ya wajumbe 200 waliohudhuria kwa njia ya ana kwa ana na pia kupitia kwa njia ya kongandao (simu ya video) kote nchini.

Kadhalika, katika mwaka huo wa 2021 tulizindua toleo la kwanza la Meat Expo and Conference, chini ya kaulimbiu ya “Nyama Salama iliyo na Ubora wa Juu kwa lishe, Afya na Uundaji wa Mali” lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa (KICC) mwishoni mwa mwaka huo. Maonyesho hayo, yaliyopangwa kwa ushirikiano na Wizara ya Mifugo, Kenya Markets Trust, Kenya Meat Commission, Baraza la Wauzaji wa Mifugo katika Masoko ya Nje ya Kenya na washirika wengine yalilenga kuchunguza suluhu inayowezekana kwa changamoto zinazokabili sekta ya nyama na hitaji la uvumbuzi, na ilituwezesha kujihusisha na kuunda mahusiano na washirika wapya katika sekta.

Awamu ya pili ya Kongamano na Maonyesho ya SME iliofanyika katika Ukumbi wa Makutano ya Kimataifa (KICC), ulileta pamoja wadau katika sekta kuangazia changamoto zinazokabili Biashara Ndogo na za Wastani (SME) nchini Kenya, kutoa jukwaa la mazungumzo ili kuleta ukuaji na kutoa fursa kwa biashara hizo kuonyesha uvumbuzi wao, chini ya kaulimbiu ya “Ustahimilivu, Kurejea na Uendelevu wa SME”. Kongamano hilo lilivutia watu 135 waliokuja kuonyesha bidhaa zao pamoja na zaidi ya washiriki 6,000.

Utambuzi wa Kimataifa

Ninajivunia kutangaza kwamba majukwaa yetu mawili ya uongozi – Nation Leadership Forum na Kusi Ideas Festival, yalishinda tuzo katika Tuzo za Kimataifa za Shirikisho la Wanahabari wa Kimataifa za 2021. Nation Leadership Forum ilituzwa kama “Bora Barani Afrika”, lilikuwa la kwanza katika kategoria ya “Matumizi Bora ya Tukio Kukuza Bidhaa Mpya”, huku Kusi Ideas Festival likiwa la pili katika kategoria hiyo hiyo. Kando na haya, kampeni ya bidhaa mpya ya Daily Nation ilituzwa nafasi ya pili kwa “Matumizi Bora ya Machapisho” huku Nation.Africa ikitajwa kwa heshima katika “Bidhaa Bora na Uvumbuzi wa Kiteknolojia”, na vilevile “Matumizi Bora ya Sauti”.

Nation.Africa pia ilituzwa kama mshindi katika kategoria za Utambulisho wa Bidhaa na Video ya Kampeni na Muundo wa Jukwaa la Kimataifa (iF) (the Oscars of Design) ikiwa ni tuzo bora kabisa katika mwaka wa kwanza tangu kuzinduliwa kwake. Tuzo hizi zimekuwa kama ushahidi kwamba tumekuza bidhaa ya kimataifa katika kipindi cha miaka mingi. Zaidi ya tuzo hizi, wafanyakazi wetu kote katika ukanda huu walitambulika kwa juhudi zao kwa kuleta habari za kuaminika katika bara hili. Mwaka wa 2021, NMG ilijishindia tuzo 9 nchini Kenya, 23 nchini Uganda na 4 nchini Tanzania.

Mabadiliko ya Utamaduni wa Kiutendakazi

Tandavu pamoja na kuharibika kwa mandhari ya vyombo vya habari kumekuwa na athari kubwa kwa wafanyikazi na maeneo yetu ya kufanyia kazi. Mwaka wa 2021, ustawi wa wafanyakazi wetu ulikuwa na jambo tulilolipa kipaumbele, kwa kukiri nafasi muhimu ambayo wafanyikazi wetu wanachukua katika kuleta mageuzi kwenye shirika. Mwaka jana, sisitizo la safari ya mageuzi ya utamaduni lilikuwa kwa utekelezaji wa matokeo ya utafiti wa utafutaji wa talanta na uboreshaji wa maarifa uliofanywa mnamo 2020.

Uchunguzi huo ulitambua mianya katika ujuzi wa kidijtali na vizingiti vilivyopo ndani ya vitengo vya biashara. Majadiliano ya makundi makinifu yaliyofanywa Kenya, Uganda na Tanzania, yalifuata utafiti huo na kutambua hatua zilizoongoza programu ya mabadiliko kwa mwaka huo na kuingia 2022. Pamoja na haya, programu ya kudhibiti mabadiliko kwa wakurugenzi wakuu nchini Kenya na Mameneja Wakurugenzi wa kampuni tanzu iliendeshwa katika Robo ya 3 ya 2021 ili kuwapa ujuzi zaidi wa kudhibiti mabadiliko na kujumuisha maadili ya NMG katika utamaduni wa kazi za kidijitali.

Nchini Kenya, Utafiti wa Maoni ya Wafanyakazi ulifanywa katika Robo ya 3 ya 2021 ili kuelewa kauli za wanfanyakazi na maeneo yanayofaa kuboreshwa kwa safari yetu ya utamaduni. Wafanyakazi wengi waliashiria kuridhishwa kwao na usawazisho uliopo wa kazi na maisha, maadili ya kibiashara, ustawi wa wafanyakazi na mafunzo.

Mwelekeo wa Kimkakati wa 2022

Kama ilivyoonyeshwa hapo juu, safari yetu ya mageuzi ya kidijitali haijafika katika kiwango tunachotarajia, lakini ni safari ambayo tumeianza kadri mabadiliko ya kiteknolojia yanavyoendelea kubadilika. Kwa hivyo, tutalitilia maanani suala hili kwenye mipango yetu ya kimkakati ya muda mfupi, kati pamoja na muda mrefu, kadri inavyohitajika, ili kushinda.

Mwaka huu, tutatilia mkazo nguzo mbili kuu, Uvumbuzi wa Bidhaa na Mabadiliko ya Kiushirika, jambo ambalo litatuwezesha kutumia majukwaa yetu yenye mikondo anuai kufanya bidhaa zetu kununuliwa, kuhusishwa na hadhira na kuchuma kutokana na maudhui. Tumetambua vigezo sita (6) vitakavyoendesha mkakati huu ifuatavyo:

 • Maudhui: Muhimu sana kwetu ni habari tunazowaletea. Hii itasalia kama nguzo muhimu ya mkakati wetu tunapoendelea kujaribu kufikia lengo letu la kuwa sauti ya wanyonge.
 • Utamaduni: Tutaendelea na ajenda yetu ya kudhibiti mabadiliko huku tukiendesha shirika shirikishi zaidi, lenye ari na linaloyapatia kipaumbele masuala ya kidijitali
 • Teknolojia: Tumewekeza katika mifumo yetu ili kuzipa hadhira zetu maudhui, kwa kuzingatia mapendeleo yao ya matumizi.
 • Talanta:
 • Wafanyakazi wetu wamekuwa ni nguzo inayosukuma ufanisi wa mkakati wetu na tutaendelea kuwekeza katika mkusanyiko wa talanta yetu ili kutoa hali ya matumizi inayoipa kipaumbele mambo ya kidijitali
 • Muundo: Tutaunda taratibu na michakato ya kazi ili kuoanisha na njia zetu mpya za kufanya kazi
 • Hadhira: NMG itatumia zana na talanta zinazotoa kiolesura na hali ya matumizi rahisi, bora inayotoa bidhaa zinazoweza kuwekwa kuzalisha chumo
 • Vigezo hivi viwezeshaji vitasababisha shirika hili kufikia sio tu lengo lake, lakini pia kukuza njia mpya za kuleta mapato ambazo hatimaye zitatoa thamani ya kijamii na kwa wadau wote.

  Kwa niaba ya Kikosi kizima cha Usimamizi Tendaji cha NMG, ningependa kuchukua fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa kila

  mshikadau ambaye anaendelea kuamini ajenda yetu ya kulea mageuzi katika jamii na kusaidia kufikia maono yetu ya kuwa Chombo za Habari cha Afrika kwa Ajili ya Afrika. Hususan, ningependa kutoa shukrani kwa wafanyikazi ndani ya NMG wanaoendelea kuonyesha ari, uvumbuzi na ustahimilivu mwaka baada ya mwingine, na kwa Bodi ya Wakurugenzi ya NMG ambao wameendelea kutoa usaidizi wao usiotetereka na kutoa mwongozo kwa biashara hii.

  Tunatazamia mwaka wa 2022 kuimarika hata zaidi, na kujitolea kuletea hadhira yetu maudhui yanayohamasisha, kufahamisha na kuelimisha. Tunapoingia katika kipindi cha uchaguzi nchini Kenya, tumejitolea kuwa kampuni yakinifu, jasiri, huru na itakayoripoti bila upendeleo na/au maonevu, na tunatazamia kutembea safari hii pamoja na wadau wetu.

  Nation Media Group
Nation Media Group