Taarifa ya Mwenyekiti

Wapendwa Wenye hisa,

Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, ninafuraha kuwapa ripoti ya utendakazi wa kifedha na usio wa kifedha wa Shirika hili kwa mwaka uliokamilika tarehe 31 Desemba 2021. Mwaka unaokaguliwa umeonyesha ishara za matumaini za kurejea kwa hali ya kawaida baada ya mwaka uliotangulia uliokuwa umejaa changamoto kwa sababu ya tandavu ya UVIKO-19 ambayo haikutarajiwa iliyoipiga dunia.

Madhara ya tandavu hii, ikijumuisha aina zake mpya, yaliendelea kuathiri watu kote Afrika kwenye ukanda wa Mashariki kupitia utekelezaji wa mchanganyiko wa hatua kama vile marufuku ya kutotembea usiku, kufungwa kwa shule katika baadhi ya nchi, huku hatua zingine za uharibifu zaidi kama vile kufungwa kwa nchi, kufungwa kwa mipaka kwa muda fulani na vikwazo vya usafiri zikiwekwa kwa awamu, na kuwekea kikomo shughuli ya kijamii na kiuchumi.

Ni kwa msingi huu ambapo uchumi wa mataifa ya Afrika Mashariki ulishuhudia ukuaji mdogo huku ukirejea baada ya kusakamwa na tandavu ya COVID-19. Biashara ilipungua katika sekta mbalimbali huku kampuni kadhaa zikipunguza idadi ya wafanyikazi wao katika sekta kama vile utalii, viwanda, uchukuzi, hoteli na malazi.

Kurejea kwa hali ya kiuchumi kwa sasa kumepigwa jeki na kuimarika kwa bei za bidhaa, kuondolewa kwa hatua kali za kudhibiti tandavu na kurejea kwa biashara ya kimataifa. Hata hivyo, hali inasalia kuwa tete kwa sababu ya viwango vya chini vya utoaji wa chanjo katika bara hili, uharibifu wa sehemu fulani za uchumi na kujikokota kwa urejesho. Benki ya Dunia inakadiria kwamba ukuaji wa 2022 na 2023 utasalia chini ya asilimia 4 tu, hii ikizidi kuvuta nyuma kasi ya urejesho katika uchumi wa nchi zilizoendelea na masoko ibuka.

Mwonekano unaendelea kuwa chanya huku kukiwa na matarajio ya kurejea kwa sekta mbalimbali kama vile ya utalii, viwanda, biashara, uchukuzi na huduma nyingine zinazotegemea utoaji wa haraka wa chanjo ili kusaidia kuzuia mawimbi mapya ya maambukizi na hatua husika za kuidhibiti. Ama kwa kweli, tumeshuhudia hatua na juhudi kubwa za watendaji wa serikali na wa sekta ya kibinafsi kote katika ukanda huu za kuhimiza shughuli za chanjo, ikijumuisha kuweka masharti ya utiifu kama matakwa ya kufikia huduma za serikali.

Katika NMG, tulichukua hatua ikiwemo kampeni kali na za kila mara za utoaji chanjo ili kulinda usalama na ustawi wa wafanyikazi wetu, familia, washirika, wateja na washikadau wengine kote katika masoko yetu yote. Shirika hili hadi kufikia sasa limetoa chanjo kwa zaidi ya 75% ya wafanyikazi wake katika masoko yake yote. Tutaendelea kusaidia serikali za ukanda huu kwa kuhimiza utoaji wa chanjo zaidi na kushirikiana na kwa ajili ya ukuaji wa sekta ya kibinafsi.

Mandhari ya Kisiasa

Nchi za Afrika Mashariki zinaendelea kupitia mpito wa kisiasa kama ilivyoshuhudiwa mwaka wa 2021. Mnamo Machi 2021, Tanzania ilipitia changamoto wakati Rais aliyekuwa madarakani John Pombe Magufuli alipoaga dunia na kurithiwa na naibu wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Mabadiliko ya uongozi yalifanyika kwa njia ya amani na rais mpya amefanya vyema katika uongozi wake. Aliweza kuleta mwafaka katika uhusiano kati ya vyama vya upinzani na baadhi ya mashirika ya kimataifa na serikali ambao wamekuwa na uhasama na Serikali kuhusu ukiukaji wa nafasi ya kidemokrasia, kufungwa jela kwa waliosuta serikali na jinsi serikali ilivyoshughulikia tandavu ya UVIKO-19. Kadhalika, alisisitiza kuunga mkono kwa dhati maendeleo ya sekta ya kibinafsi, ambayo imeimarika katika uhusiano wake na serikali.

Jirani yake upande wa Kaskazini, Kenya, inatarajia kuenda katika uchaguzi Mkuu mwezi Agosti 2022 ambapo rais mpya anatarajiwa kuchukua uongozi. Pia kuna uchaguzi katika nyadhifa za Ugavana, wabunge na nyadhifa nyinginezo. Baadhi ya wasiwasi katika kampeni kufikia sasa ni pamoja na kuibuka kwa idadi kubwa ya vijana wapiga kura ambao wamegawanyika, kujikokota kwa maandalizi ya miundomsingi ya uchaguzi kama vile sheria, na kuzidi kupanda kwa joto la kisiasa, ikijumuisha matamshi ya chuki, uchochezi na matukio mengi ya kutoifahamisha umma.

Ili kukabiliana na changamoto hizi, Kampuni imechukua nafasi yake katika uhamasishaji wa umma kuhusu masuala muhimu kwa kutoa mwito wa kuunganisha wananchi kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Kutokana na hili, NMG ilizindua mpango wa “Mimi Mkenya”, unaolenga kuhimiza uzalendo, uchaguzi uliojikita katika masuala muhimu, amani na umoja kuanzia katika ngazi ya mashinani na kusambaa kote nchini. Kampeni hii inalenga kudumisha dhana ya umiliki na uwajibikaji miongoni mwa Wakenya na washikadau wengine kutoka biashara, washirika wa maendeleo, asasi za kitaifa na marafiki wa Kenya na washikadau wengine wote kufanya kazi pamoja kuhakikisha kuna uchaguzi wa amani Agosti 2022.

Kupitia mpango wa Mimi Mkenya, Shirika hili limesisitiza kujitolea kwake kutekeleza sera ya uhariri ili kuwahudumia wawaniaji wote kwa usawa, kwa uyakinifu lakini bila woga; kutoa jukwaa kwa kila mtu ambaye angependa kuchukua fursa, kuwajibisha viongozi kwa seti ya masuala muhimu kwa nchi na wananchi kupitia mpango wake wa Nation Agenda (NMG imekuza nyanja kuu za kuendesha kampeni zilizojikita katika masuala muhimu kuhusu mambo ya maslahi ya umma). Kadhalika, tutapigana bila woga dhidi ya uchochezi, matamshi ya chuki na hali ya kutoifahamisha jamii, kushirikisha vijana na kuwapa jukwaa la kujadili masuala yao na kuchunguza ukweli wa yale viongozi wanasema na kusuta watu wanaokosa kuifahamisha jamii, mambo yasiyo sahihi na kufungia nje mambo mengine kwa kukusudia.

Matokeo ya Kifedha

Shirika hili lilipata mauzo ya shilingi bilioni 7.6 na faida ya kabla ya kodi ya shilingi bilioni 0.7, na kusajili kuimarika ikilinganishwa na 2020 ambapo tulipata shilingi bilioni 6.8 na faida ya shilingi bilioni 0.1 mtawalia. Kurejea kwa biashara kulitokana na kufunguliwa tena kwa sekta nyingi za uchumi na kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo vilivyohusiana na tandavu hii kama vile kufungwa kwa nchi. Shirika hili lilisajili ukuaji mkubwa kwa sababu ya kushika kasi kwa mipango ya kidijitali, kurejea kwa mapato kutokana na televisheni na machapisho. Pamoja na hayo, hatua zilizolenga kudhibiti gharama zilichukuliwa ili kuimarisha ufanisi wa utendakazi na kuongeza tija.

Mgao

Licha ya mazingira ya kiuchumi yenye changamoto, biashara inarejea polepole baada ya madhara ya tandavu iliyoipiga dunia. Wakurugenzi wanapendekeza malipo ya mgao wa mwisho wa mapato ya hisa wa Shs 1.50 kwa kila hisa kwa mtaji wa hisa uliotolewa na uliolipiwa kufikia tarehe 31 Desemba 2021, bila kujumuisha hisa za hazina ya kitaifa zilizonunuliwa tena katika mwaka huo. Hakuna mgao wa mapato ya hisa ya muda uliolipwa katika mwaka huu.

Ununuaji Upya wa Hisa

Wakati wa Mkutano Mkuu wa Kila Mwaka (AGM) uliofanywa tarehe 25 Juni 2021, Wenye hisa waliidhinisha Ununuaji Upya wa Hisa wa hadi asilimia kumi (10%) wa hisa zake za mtaji zilizokuwa zimetolewa na kulipiwa kwa bei bora ya Shs 25 kwa kila hisa kwa mujibu wa vipengee vya Sheria ya Kampuni (2015) vya Sheria ya Kenya. Hii iliwapa wenye hisa fursa ya kuchuma pesa taslimu kutokana na uwekezaji wao. Ununuaji Upya wa hisa ulifungwa tarehe 24, Septemba, 2021 huku ikikumbatiwa kwa namna ya kuridhisha kwa 82.45% (hisa milioni 17.1) Hisa zilizonunuliwa tena zinahifadhiwa na kampuni kama Hisa za Hazina.

Safari ya Mageuzi ya Kidijitali

Safari ya mageuzi ya kidjitali ya Kampuni imekuwa ya kutia moyo huku 2021 ukishuhudia kupigwa kwa hatua kubwa katika mwanzo wa safari ya kubadili muundo wake wa biashara kuwa ule ambao ni mseto huku mapato kutokana na machapisho na usomaji yakiwa ni nguzo kuu zilizoendeshwa na maudhui ya kidijitali huku pia ikichunguza njia mpya za kuleta mapato katika nyanja za matukio na teknolojia.

Mnamo Februari 2021, NMG ilikuwa kampuni ya kwanza ya habari katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuzindua huduma ya kujisajili inayolipiwa kwa ajili ya maudhui yake ya kidijitali. Kwa kuzingatia kuwa hii ni safari ngeni tumejipata kwayo, tunafurahishwa na hatua tuliyoipiga kuhusiana na ukuaji muhimu katika kupata hadhira kupitia watu kujiandikisha na kulipia usajili, upanuzi wa maudhui ya kuvutia yanayohusu bara la Afrika na kuboresha miundo yetu ya maudhui kwa miundo mipya ya habari kama vile podikasti, mafumbo, video na majarida.

Uongozi katika Mawazo Pevu

Shirika hili linaendelea kutumia uwezo wake wa kuleta watu pamoja ili kukuza taswira ya maendeleo na mustakabali wa ukanda huu na Afrika kupitia majukwaa yake yanayolenga nchi mahususi na ya Afrika nzima. Tuliandaa misururu ya Mijadala ya Nation Leadership Forums (NLF) na Mwananchi Thought Leadership Forums nchini Tanzania. Mijadala hii ya mazungumzo ilijadili kwa kina nyanja muhimu kama vile kilimo, afya, SME, viwanda, elimu, teknolojia, utozaji wa kodi miongoni mwa mengine na kuleta pamoja wataalamu anuwai kujadili masuala ibuka yanayoathiri ukanda huu. Maono ya NMG ya kuwa ‘Chombo cha Afrika kwa Ajili ya Afrika’ yaliimarishwa wakati iliandaa awamu ya tatu ya Tamasha ya Kusi Ideas, kule Afrika Magharibi - Accra, Ghana mwezi Desemba 2021. Kuanzia Kusi I (Kigali, Rwanda) hadi Kusi II (Kisumu, Kenya), hali mpya ya dharura iliingizwa katika mazungumzo kuhusu mawazo ya kujenga Afrika nzima na awamu hii inalenga kukagua umuhimu wa ushirikiano wa kibara, chini ya kaulimbiu ya “How Africa Transforms Under the Virus”.

Eneo lililochaguliwa kwa ajili ya awamu ya tatu ya tamasha hii lilikuwa la aina yake kwa kuwa Accra ndipo palipo Makao Makuu ya Eneo la Biashara Huru la Bara la Afrika (AfCFTA), hivyo kutoa ukumbi bomba wa kujadili mada ya 2021.

Kongamano hilo lilivutia wazungumzaji 34, kutoka kote barani Afrika na vilevile wasemaji wa kimataifa wenye masilahi yao na kutumia ujuzi wao ndani ya bara hili. Awamu ya tatu ya Kusi Ideas Festival iliandaliwa kwa pamoja na Mheshimiwa Rais Nana Akufo-Addo, Rais wa Jamhuri ya Ghana na kuvutia washiriki kuanzia Mheshimiwa Rais Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Rais Yoweri Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Rebecca Grnyspan, Katibu Mkuu wa Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD); Mheshimiwa Wamkele Mane, Katibu Mkuu, AfCFTA, Mheshimiwa Dkt. Peter Mathuki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, miongoni mwa washikadau wengine ikijumuisha wataalamu, wavumbuzi, wasomi, wajasiriamali, viongozi wa tasnia na wawakilishi kutoka katika jumuiya ya mabalozi. Wajumbe 1,080 walihudhuria ana kwa ana, wajumbe 17,000 kupitia simu ya video kutoka nchi 72 na miji 401 na ilivutia zaidi ya hisia milioni 200 kwenye mitandao ya kijamii.

Ajenda ya Uendelevu

Shirika hili linalenga kujenga biashara endelevu kwa sababu siku zijazo ni za umuhimu sana kufuatia yale tuliyojifunza kutokana na tandavu ya COVID-19. Biashara yetu itazalisha na kutoa thamani tu ikiwa itadumisha juhudi zake za kudumisha matendo endelevu ya biashara kwenye utendaji kazi wake wote na kutilia maanani masuala ya kimazingira, kijamii na utawala. Shirika hili lina taratibu thabiti za uongozi ikijumuisha mwelekeo oanifu wa kusimamia nyenzo muhimu za hatari kwa biashara ikiwa na utaratibu wazi wa ufuatiliaji na kushirikisha wahusika wa ngazi za juu.

Nimehimizwa kupitia juhudi za NMG katika kuchukua nafasi muhimu katika uendelevu wa kimazingira. Shirika hili limeanzisha jarida linaloitwa ‘Climate Action: Why it Matters Campaign’ linalowaleta pamoja wataalamu wa mazingira kuendesha mazungumzo muhimu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Jarida hili limetambuliwa kimataifa katika Tuzo za INMA World Media za mwaka wa 2021. Ni kujitolea huku kulikofanya Shirika kuchukua nafasi ya kuleta watu pamoja ili kuhusisha Kenya katika kujadili nafasi za mabadiliko ya hali ya hewa kwa kujiandaa kwa ajili ya COP26. Isitoshe, Shirika pia lilifanya ushirikiano wa kimkakati katika mipango muhimu ya kimazingira kama vile kuanza kutumia vitalu kulinda maeneo yenye chemchemi za maji katika Kaunti za Uasin Gishu na Machakos. Tunajitolea kuongeza shughuli hizi huku tukichukua nafasi ya kuleta wadau pamoja ili kushirikisha washirika zaidi na kuendesha kampeni ya mabadiliko kupitia majukwaa yetu yote ya habari.

NMG kote katika ukanda huu inaendelea kuunda na kutekeleza mipango yenye athari ya kijamii katika nyanja kama vile afya, elimu, mazingira, msaada wakati wa janga na maendeleo ya jamii. Kutokana na hayo, Kampuni hii imesajili ‘Wakfu wa Nation Media’ ili kuiwezesha kutuma rasilimali na kuvutia ushirikiano muhimu wa kimkakati utakaosababisha upanuzi wa mipango ya Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs). Hii itakuwa ni chombo muhimu cha kubuni thamani ya pamoja kwa wenye hisa na washikadau.

Mabadiliko kwenye Bodi

Kulikuwa na mabadiliko kwenye Bodi mnamo mwaka jana. Prof. Samuel Sejjaaka aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Asiye Mtendaji na Mwenyekiti wa kampuni tanzu nchini Uganda, Monitor Publications Limited mnamo Januari 2022. Hii ilifuatia kifo cha Dkt. Simon Kagugube mwaka wa 2021. Bodi itanufaika pakubwa kutokana na tajriba yake pana katika usimamizi, usimamizi wa utawala katika kampuni za maslahi

Watu Wetu

Mageuzi ya kidijitali ya Shirika yatafanyika, si tu kupitia teknolojia bali hususan kupitia kikosi cha wafanyikazi wenye ujuzi anuwai, wanaojituma na wenye uwezo wa kubadilika ipasavyo. Kutokana na haya, lengo la NMG lipo katika kukuza uwezo wake wa kindani kupitia kuipa timu ya sasa ujuzi upya na ujuzi zaidi huku vilevile ikitafuta ujuzi mpya

Mustakabali wa Siku za Usoni

Katika mwaka mmoja ujao, Shirika linatambua fursa za kipekee na changamoto zilizopo katika uwanja wa kidijitali. Tunaendelea kujifunza mambo muhimu ambayo ndiyo msingi wa kuendelea kwetu kufanya uvumbuzi na kuboresha tunapotazamia kufikia sifa ya kimakakati ya Nyota wa Kaskazini ya kuwa kampuni ya maudhui ya kisasa ya kidijitali. Kwa hivyo, lengo litakuwa ni kuongeza kasi ya bidhaa zilizopo katika nyanja za kidijitali ili kuimarisha ukuaji katika njia mpya za mapato na hadhira.

Ili kutuwezesha kufanikiwa, tunaendelea kukuza bidhaa mpya, kuwekeza na kuingia katika ushirikiano muhimu wa kimkakati, teknolojia na talanta. Mwisho, tutatambua fursa za kuungana na ununuzi wa bidhaa zitakazosaidia Shirika hili kuongeza thamani katika nyanja muhimu za athari ya kijamii kama vile kilimo, vijana, mazingira, elimu, teknolojia miongoni mwa mengine. Hii itajumuisha kuchunguza uwezekano wa kuingia katika masoko mapya ibuka kama vile Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Nigeria, Malawi na Ghana.

Bodi imefurahishwa na hatua ambazo usimamizi na wafanyikazi wamechukua, wakati wa kipindi kigumu ili kufanya Shirika kuwa katika njia ya kurejea katika hali ya kawaida. Bodi imeridhishwa na mwonekano wa kimkakati wa kampuni na mipango iliyopo ya kuendelea kulinda NMG kama biashara endelevu. Nachukua fursa hii kushukuru wakurugenzi wenzangu kwenye Bodi kwa kujitolea kwao, ari yao na ushauri wao wenye busara. Ninashukuru kwa dhati mchango wao muhimu wakati ambapo uongozi ulihitajika ili kuongoza dau hili kwenye maji yaliyokuwa na mawimbi makali.

Yote tisa, kumi ni kwamba kurejea kwa hali ya kawaida iliyoshuhudiwa haingewezekana bila usimamizi na wafanyikazi wa NMG kutia bidii, juhudi zisizotetereka, ufanisi na kufanya kazi kama timu. Shukrani zangu za dhati sana ziwafikie nyote. Ninashukuru kila mmoja wenu kwa kuwa balozi wa lengo letu, kushiriki mtazamo wa pamoja, kwa kutumia seti ya maadili inayotuongoza. Shukrani zangu za dhati kwa kuendelea kusaidia washirika wetu wa biashara, wateja wetu na washikadau wengine.

Ahsanteni sana!
Nation Media Group
Nation Media Group